Kuwa mtumishi

Niliulizwa nilipowekwa kuwa padre, “Ni mstari gani katika Injili unaongoza maisha yako?” Nilijibu mara moja, “Nenda upande wa pili na upige nyavu zako!” Nihiyo iliyoniongoza katika miaka ya kwanza ya upadri wangu: kuwaendea wengine, kukutana nao. Na kadri walivyokuwa maskini, ndivyo nilivyotamani kukutana nao zaidi, nilitaka kuunganisha maisha yangu na yao. Lakini niligundua kuwa kimsingi hakuwa lazima kuwa mtumishi kwa maana kamili ya neno hilo, yaani mtu ambaye anategemea kabisa amri ya bwana. Kwa hivyo, si kwa sababu nilikuwa kati ya maskini, kuteseka na baridi kama wao na kukosa mkate kama wao, humaanisha nilikuwa kweli mtumishi wa watu hawa wenye dhiki nilioishi nao. Nilikuwa na ulinzi wangu. Nilikuwa na utu wangu pia. Nilikuwa na yale niliyoyapata katika seminari, na nyuma yangu kulikuwa na kanisa lote. Naweza kukosa mkate katika mtaa wa mabanda, lakini nilijua kwamba siku ambayo ningetaka… kulikuwa bado na Kanisa lenye nguvu nyuma yangu.

Kuwa mtumishi si rahisi kama tunavyoweza kufikiria. Kwa sababu daima tunakuwa na akiba na biskuti kwenye mfuko.

Kimsingi, nimegundua katika maisha yangu kama padri, maisha yangu katikati ya watu na maskini, kwamba singeweza kuwa mtumishi wa kweli kwa yeyote kati yao isipokuwa kwanza kuwa mtumishi wa wale ambao walikuwa wananifikia, ambao walikubali kuacha hali yao ili kuwa watu waku jitolea katika Harakati ya ATD Dunia ya Nne, waliogeuka kuwa marafiki zangu. Siku nilipofahamu hilo, huwezi hata kuwazia jinsi nilivyohisi kuwa huru.

Kwa sababu, nilipokuwa nimejitosa moyoni mwa umaskini, nilikuwa najifikiria kimoyomoyo, lakini sikuthubutu kuusema: “Mimi ni mtu mkubwa, mimi ni mtu mzuri, nafanya mambo mengi sana!”

Siku niliyogundua kuwa wale ambao wangeweza kunifundisha kuwa mtumishi siyo maskini, bali ni wale ambao walihitaji kujitayarisha, kukua, na kujifunza ili kuishi moyoni mwa umaskini, hilo lilikuwa ni ukombozi wa ajabu. Tangu wakati huo, niliamini kwamba watu wote, si tu wanaweza kuokolewa, bali wanaweza kuwa wokovu.

Hii ilikuwa ya ajabu, mapinduzi makubwa ndani yangu. Niligundua kuwa naweza kuwa na imani kubwa kabisa kwa wengine. Kimsingi, niliwafahamu kwa njia ya utumishi, kwa kuosha miguu. Niliwafahamu wakati walikuwa na matatizo ya kiroho, kihisia, kimwili, kiafya, au vinginevyo. Niliwafahamu wakati wa shauku kubwa na pia wakati wa kurudi nyuma kwa kishindo.

Niliwafahamu katika udhaifu wao, na pia katika ujasiri wao. Naweza kusema kwamba niliwaingiza katika maisha yangu, moyoni mwangu, kama wao ndiyo watu pekee wenye umuhimu kwangu. Ndio maana, katika kipindi cha miaka kumi na tano iliyopita, nimejitolea kabisa kukutana nao, nadhani sio tu kutoa mafunzo kwao, kwa watu waku jitolea ambao wanaishi katika ulimwengu, katika maeneo ya umaskini. Najiambia kuwa mimi ni mtu huru kwa sababu naamini kwao, na nina hakika yakwamba wote wanaitwa kuwa wakombozi, sisi sote tunaitwa kuwa hivyo. Kwa sharti la kujifunza kwanza kutumikia wale waliokuwa karibu nawe, kuwatumikia kwa vitendo, siyo tu kwa maneno, lakini kwa njia ambayo maisha yako yote yatabadilika na kugeuzwa kabisa.

0 comments Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.