Mama alitufundisha kujivunia hali yetu

Nilianza kufanya kazi nikiwa na umri wa miaka minne.

Nilikuwa na umri wa miaka minne nilipoanza kufanyakazi ili kujipatia riziki kwa kuhudumia ibada ya misa. Kwa upande wangu, hakika hii ilikuwa ni kazi kwa sababu nilikuwa ninalipwa kwa kupewa cho chote cha kuweka kinywani kila baada ya ibada ya asubuhi: bilauri kubwa la kahawa ya maziwa na mkate. Siku za Jumapili nilipewa mkate uliopakwa siagi vile vile kila juma tulipewa pesa kidogo.

Ni Sista Augustine aliyenisaidia kupata hii kazi. Kila siku alikuwa akituangalia mimi na kaka yangu tulipokuwa tukitelemka na mbuzi wetu kwenda machungani. Uwepo kwa huyu mbuzi ulimhakikishia mdogo wetu uhakika wa kupata walao maziwa kidogo. Sista Augustine aliwekea maanani sana afya ya mdogo wangu wa kike na pia alimjali sana mama yangu. Alifanya urafiki na sisi kwa kuwa tulikuwa watoto maskini.

Shomoro wetu alikufa.

Nakumbuka wakati nilipokuwa mdogo, mimi na kaka yangu tuliokota mtaani ndege aliyekuwa amejeruhiwa, tukamleta nyumbani. Tulimweka katika tundu na kumlisha. Tulimpatia maji na kumtunza vizuri. Hakika tulimpenda sana. Mama alimfurahia sana namna alivyokuwa akiimba.

Lakini baadaye mambo yalituendea kombo kabisa. Baba alikata mawasiliano na nyumbani hatukuwa na fedha. Hapakuwa na chochote kabisa. Mama alizama katika dimbwi kubwa la majonzi nasi wanaye tulilia sana. Hatukuelewa nini kilichokuwa kinaendelea na pia hatukufahamu tufanye nini. Niliamua kuiba maua nikampelekea mama nikitarajia kwamba yatamchangamsha. Niliomba fedha kwa mmiliki wa bucha ili niweze kumnunulia chochote lakini hakuna kilichoweza kumchangamsha.

Siku moja mambo yalibadilika na jua liling’ara tena. Hapo ndipo tulipogundua kwamba shomoro wetu alikuwa haimbi tena. Alikuwa amekufa. Katika matatizo yetu, tulikuwa tumemsahau.

Hivyo ndivyo taabu za kibinadamu zinavyoweza kukufanya: kamwe huwezi kuwa na uhakika wa kuwashikilia uwapendao.

Mama alitufundisha kujivunia hali yetu

Wakati fulani hali ilikuwa mbaya sana kiasi kwamba mama alishauriwa anipeleke katika makazi ya yatima. Majirani walishauri kwamba huko nitaweza kujifunza ujuzi wa kazi yo yote. Pamoja na hayo, nilikuwa mtoto nisiyevumilika. Nilikuwa mwizi wa mapeazi kwa majirani na nilikuwa mdanganyifu kupita kiasi. Nakumbuka siku moja nilivyokwenda katika mgahawa mmoja ambamo mlikuwa mnauzwa sigara, nikachomoa bastola iliyokuwa na risasi za mpira na kupiga kelele nikisema “Mikono juu!” Kisha nilizoa pesa yote iliyokuwa juu ya meza. Kusema kweli nilikuwa mtoto mtukutu sana katika maeneo yote ya jirani na kila wakati nilijikuta katika matatizo ya kila namna.

Kama leo hii ningerejea katika hali yangu ya utoto nikiwa na tabia yangu ile, kwa namna jamii ya sasa ilivyo, hakika ningelipelekwa katika shule ya kurekebisha tabia. Ilivyokuwa ni kwamba jirani zangu hawakupendezwa na tabia yangu na wakati mwingine nilimweka mama katika matatizo makubwa sana. Mama alihofia sana kuhusu kuharibika kwa sifa njema ya familia tetu, hivyo watu walimshauri anipeleke katika nyumba ya yatima. Kila mtu alipendekeza hivyo. Usiku ule nilipokuwa najiandaa kuondoka, mama alitamka, “Hapana haiwezekani, wewe si yatima, unaye mama wewe!’

Kwa kweli ni mama yangu ndiye aliyenifanya nijihusishe na familia zinazoishi katika lindi la umaskini. Baba yangu aliondoka nyumbani kwenda kutafuta kazi, hivyo mama yangu alibaki peke yake pamoja na watoto wanne. Hata hivyo tunamshukuru mama kwamba hatukuwa na majonzi ingawa mara kwa mara tulidhalilishwa, Iakini mara zote mama yetu alifahamu namna ya kutufanya tujisikie vizuri tena. Tunashukuru kwamba kwa jinsi hiyo tulikuwa na utambulisho, kwamba tulikuwa watu fulani katika mazingira yetu. Watu walizoea kutuita kwa jina la “Akina-Kiki”, ambalo ni jina la ukoo wetu.

Hata katika hali yake ya ufukara, daima mama kwa namna moja ama nyingine alipata msaada kwa sababu alilinda heshima yake na kujivunia hali yake. Daima alitufundisha kuona fahari katika hali yetu. Endapo mtu yeyote alionesha hali ya kutudharau, mama hakusita kumkemea akisema, “Kamwe sikubaliani na hilo!” Hivyo, watu walituheshimu.

0 comments Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.